Call: +255 22 2668992

VIONGOZI WAPYA OUT WAHIMIZWA KUFANYA KAZI KWA WELEDI NA USHIRIKIANO.

viongozi-wapya-out-wahimizwa-kufanya-kazi-kwa-weledi-na-ushirikiano

Menejimenti ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) yaaswa kutumikia nyadhifa zao kwa weledi na kwa kushirikiana na mamlaka husika zilizopo chini na juu yao katika kuchukua ushauri na maoni ili kuiendesha taasisi kwa weledi kwa kufuata miongozo na sheria zilizowekwa kukiongoza chuo.

Akizungumza katika hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi kutoka viongozi wanaomaliza muda wao kwenda kwa viongozi wapya, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Prof. Elifas Tozo Bisanda, amesema tukio hili ni zuri kwani linasaidia kudumisha mahusiano mema kati ya uongozi unaotoka na uongozi unaoingia.

“Cheo ni dhamana na kwa maana hiyo tunashikilia mamlaka tunayopewa kwa muda na kuyaachia pale muda unapokuwa umekwisha. Tupo katika mfumo wa kiuendeshaji wa kupokezana vijiti vya nafasi za uongozi, nawashukuru Prof. Deus Ngaruko na Prof. George Oreku ambao wanamaliza muda wao, nimekuwa nikishirikiana nao sana katika kuiendesha taasisi wakinishauri na kunisaidia utekelezaji wa majukumu hivyo ni nguvu kazi ambayo kwangu ilikuwa na msaada mkubwa na kunifanya nijisikie ugumu kuiachia ila kwa taratibu za uongozi wa utumishi wa umma katika vyuo Vikuu inabidi iwe hivyo” amesema Prof. Bisanda.

Aidha, ameendelea kwa kuwapongeza viongozi wapya walioteuliwa, Prof. Alex Makulilo ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayesimamia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu na Prof. Josiah Katani ambaye ameteuliwa kushika nafasi ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayesimamia Mipango, Fedha na Utawala. Prof. Bisanda, amewaasa kuwa nafasi hizo sio nafasi rahisi lakini utumishi wa umma ni kujitoa, hivyo kwa kushikirikiana na mamlaka saidizi kwao ni matarajio kuwa kazi zitakwenda vizuri.

Akiongea katika hafla hiyo Prof. Deus Ngaruko, amewashukuru watumishi wote hasa aliofanya nao kazi kwa ukaribu kwa ushirikiano alioupata kwa kipindi chote cha uongozi wake kama Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu) na kuwatakia kila la kheri viongozi wapya waliopewa dhamana ya kuliendeleza gurudumu hilo.

“Kazi yangu ilikuwa rahisi kwani nilikuwa nafanya kazi na watu ninaoelewana nao sana . Nilikuwa na timu nzuri ya wakuu wa Vitivo, Wakurugenzi, Wakuu wa vitengo na Wakuu wa idara hivyo hata kazi ngumu niliyokuwa nayo kwangu ilikuwa rahisi,” amesema Prof. Ngaruko.

Naye Prof. George Oreku, amemshukuru Makamu Mkuu wa Chuo na mamlaka ya uteuzi kwa kumwamini na kumpa nafasi hiyo kubwa na kusema katika uongozi haijalishi ni kwa muda gani utakaa kwenye nafasi ya uongozi bali ni nini unafanya wakati ukiwa kwenye uongozi.

“Hivyo nawapongeza walioteuliwa katika nafasi hizi za uongozi, tupo hapa hapa chuoni tunarudi idarani kuendelea kufundisha na  tutatoa ushirikiano na ushauri kwa viongozi wapya na Menejimenti kwa jumla pale itakapohitajika, nafasi hizi za uongozi sio rahisi lakini kwa kumtanguliza Mungu na kushirikiana na watumishi wenzetu mambo yatakwenda sawa,” amesema Prof. Oreku.

Akiongea baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Prof. Makulilo, amesema “Nashukuru mamlaka ya uteuzi kwa kuniamini na kuniteua niweze kuitumikia jumuiya ya OUT kupitia nafasi hii. Pia ninaahidi kuendeleza pale Prof. Ngaruko alipoishia kikubwa naomba ushirikiano wenu uendelee kama ulivyokuwa kwa uongozi uliopita”.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayesimamia Mipango, Fedha na Utawala, ameshukuru kwa imani aliyopewa na kuwa mmoja wa familia ya chuo hiki. “Natambua ofisi hii ni sehemu inayogusa maslahi ya wafanyakazi, hivyo tushirikiane ili mambo yaweze kwenda kama tunavyotarajia,” amesema Prof. Katani.

Akihitimisha hafla hiyo, Katibu wa Baraza la Chuo na Mwanasheria wa chuo, Wakili Nelly Moshi, amewapongeza viongozi wote waliomaliza muda wao kwa utumishi uliotukuka na kuwakumbusha kuwa wao ni hazina ya chuo hiki hivyo wasichoke watakapohitajika kwa ushauri. Amewaasa viongozi wapya kujituma na kuwa wabunifu zaidi katika kazi zao kwa lengo la kuendeleza mambo makubwa na mazuri yaliyofanywa na viongozi waliomaliza muda wao na pia kubuni mambo mapya zaidi kwa ustawi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Hafla hii fupi ya makabidhiano ya ofisi imefanyika katika makao Makuu ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyopo Kinondoni jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na viongozi waandamizi pamoja na watumishi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).