UZINDUZI WA BARAZA LA KUMI LA WAFANYAKAZI OUT – BABATI
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mh. Queen Cuthbert Sendiga, amelitaka Baraza Kuu la Wafanyakazi la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kujadili mambo yenye tija yatayosaidia kuongeza udahili na mapato ya chuo ili kujiimarisha zaidi katika utoaji wa huduma zake.
Mh. Sendiga, ametoa rai hiyo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Baraza la Kumi la Wafanyakazi wa OUT linalofanyika leo (Machi 15, 2024) mjini Babati mkoani Manyara ambapo amewataka wajumbe hao kukishauri chuo kujikita zaidi katika tafiti zenye kuleta tija kwa nchi.
“Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni chuo pekee nchini kinachoweza kufikia Watanzania wengi kwa wakati mmoja, hii ni kwa sababu kimeweza kusogea mpaka ngazi ya wilaya, ongezeni vituo zaidi ili kuwafikia wafanyakazi wanapokuwa kazini huku wakijiendeleza kimasomo bila kuvuruga ratiba zao za kazi.” Amesema Mh. Sendiga.
Pia Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Elifas Bisanda, ameeleza mpango wa chuo katika kutafuta rasilimali fedha ili kuwawezesha wahadhiri wa OUT kwenda maeneo ya vijijini kufanya tafiti zitakazowezesha chuo kuleta mabadiliko kwa jamii hasa kuongeza ubora katika uzalishaji.
“Ili kumletea mwananchi maendeleo chuo kimetoa ufadhili kwa waratibu kata ambapo akifanikiwa kuleta wanafunzi kumi anapata ufadhili wa masomo katika chuo hiki kwa mwaka mzima. Tunahimiza waratibu kata wote kujiunga katika mradi huu ili nao waweze kujiendeleza kielimu na kuboresha utendaji katika ngazi za chini za maamuzi.” Amesema Prof. Bisanda.
Akihitimisha ufunguzi wa Baraza hilo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayesimamia Taaluma, Tafiti na Huduma za kitaalamu, Prof. Deus Ngaruko, amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuitikia wito wa kulifungua Baraza na kuahidi kufanyia kazi yale yote yaliyoshauriwa ili kulifanya Baraza kuwa kitovu cha kutengeneza hoja na mikakati itakayolenga kuongeza maslahi ya watumishi, uadilifu na ufanisi wa shughuli za chuo.