Call: +255 22 2668992

PROF. NGARUKO: OUT IMEPIGA HATUA KUBWA UTEKELEZAJI WA MRADI WA HEET

prof-ngaruko-out-imepiga-hatua-kubwa-utekelezaji-wa-mradi-wa-heet

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kimepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa mradi HEET ambapo katika maeneo yote yanayohusu mradi huo kazi zinaendelea kutekelezwa kikamilifu.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri elekezi Prof. Deus Ngaruko ambaye pia ni mratibu Mkuu wa mradi wa HEET kichuo, ameyasema hayo kwenye kikao kazi cha siku mbili kuanzia Novemba 11 na 12 Novemba, 2023 wakati akitoa ripoti ya utekelezaji wa mradi kwa wativa, wakurugenzi, wakuu wa idara na vitengo vya OUT mjini Bagamoyo mkoa wa Pwani.

“OUT imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa mradi wa HEET na mnapaswa kufahamu na kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa mradi hatua kwa hatua ili pale tunapopata changamoto tunaitatua kwa pamoja. Tayari kwa upande wa kusomesha wanataaluma katika ngazi za Umahiri na Uzamivu tumeshapeleka wahadhiri 23 kati ya 24 tuliopangiwa. Kwa upande wa ujenzi ya maabara za sayansi tumeshafanya tathimini ya mazingira na masuala ya kijamii, mshauri elekezi wa mradi keshapatikana na kazi inayofuata ni kuwapata wakandarasi wa kujenga maabara hizo katika kanda saba (7) za OUT.” Amesema Prof. Ngaruko.

Prof. Ngaruko ameongeza kuwa, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inayosimamia utekelezaji wa mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya kiuchumi nchini (HEET), kimekuja na mradi wa uwekezaji wa kituo cha Utafiti, Ubunifu na Ugundizi (ORIC). Kituo hicho kitachojengwa Bungo mjini Kibaha na kitasheheni viwanda, mashamba, mabwawa ya samaki na utakatishaji majitaka, mifugo, majiko na maabara za kisasa za sayansi na utalii zitakazotumiwa katika tafiti na mafunzo kwa vitendo.

“Kituo cha ORIC, kitakuwa na miradi mbalimbali ya uwekezaji. Wanafunzi na wahadhiri wa chuo hiki, watafanya tafiti zao moja kwa moja ili kuja na majawabu yenye kutatua changamoto za jamii katika shughuli za maendeleo. Wanafunzi wa mazoezi kwa vitendo, kazi za kujitolea na wasio na uwezo wa kujilipia ada watafanya kazi za uendeshaji wa kituo na kupata kipato kitakachowasaidia kimasomo. Wabobezi na wanasayansi kutoka taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi pia watakaribishwa kutumia kituo hicho kwenye kazi zao za kitaaluma na kiutafiti.” Amesema Prof. Ngaruko.

Naibu mratibu wa mradi, Dkt. Timoth Lyanga, akitoa taarifa za utekelezaji wa mradi wa HEET amesema mradi unaendelea vyema na sasa kinachofanyika ni kuhitimishwa kwa zoezi la tathmini za kimazingira na masuala ya kijamii (ESIA). Wakati huo huo mchakato wa kuwapata wakandarasi watakaojenga majengo ya maabara saba za kikanda ukiwa unaendelea vyema.

Kwa upande wake mratibu wa mradi katika kipengele cha kuwaendeleza wanataaluma na upitiaji wa mitaala Dkt. Yohana Lawi, amesema kuwa nafasi ya ufadhili imebaki moja tu. Imebaki kwa wanataaluma kwenda masomoni na nafasi nyingine zote zimeshapata wahadhiri ambao wapo masomoni tayari. Kwa upande wa mitaala kazi mbili kubwa tayari zimekamilika ambapo ni kuwatafuta wahitimu (Tracer study) na kujua mahitaji ya soko (Market survey). Kazi inayoendelea ni idara na vitivo kuitisha mikutano ya wadau na kuwasilisha mitaala husika kwenye vyombo vya maamuzi katika ngazi ya chuo.

Aidha, mradi wa HEET unatoa ufadhili kwa wasichana na wanawake 1000 wenye sifa za kujiunga na mafunzo ya awali ya msingi (Foundation Program) katika michepuo ya Sayansi, Injinia, Teknolojia na Hesabu waliopitia changamoto mbalimbali zikiwemo kupata ujauzito wakiwa masomoni, umasikini, ukatili wa kijinsia na changamoto za maisha kwa jumla na hivyo kuwasababishia kukatisha masomo yao.  Katika awamu ya kwanza wanafunzi 141 wamepokelewa na wanaendelea na masomo kwa kufadhiliwa kila kitu ikiwemo ada, malazi, nauli, bando na vishikwambi kwa ajili ya kujisomea.

Hivyo, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinatoa wito kwa wasichana na wanawake wote wenye sifa stahiki kutembelea tovuti ya chuo hiki ya www.out.ac.tz ama kufika kwenye vituo vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania vilivyopo katika mikoa yote Tanzania Bara na Unguja na Pemba Tanzania Zanzibar ili kupata taarifa zaidi na kufanya maombi kwa ajili ya awamu ya pili kabla ya Novemba 30, 2023.