Mkuu wa wilaya ya Mbeya, Mh. Beno Malisa, ametoa pongezi kwa Chuo Kikuu Huria cha Zanzania(OUT) pamoja na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kushirikiana kuandaa na kuendesha makongamano yenye lengo la kutangazia vivutio vya utalii wa anga vinavyopatikana mkoani Songwe.
Mh. Malisa, ametanabaisha hayo wakati akizindua kongamano la pili la utalii wa anga leo Juni 29, 2023, lilifanyika katika ukumbi wa hotel ya GR Comfort katika manispaa ya Mbeya ikiwa ni muendelezo wa shughuli mbalimbali kuelekea maadhimisho ya siku ya kimondo duniani Juni 30.
“Lengo la kongamano hili ni kuhamasisha utalii wa anga na malikale kama utalii adhimu nchini na kwa upande wa nyanda za juu kusini kipo kimondo kinachopatikana Songwe ambacho ni kiashiria halisi cha utalii wa anga katika ukanda huu. Natoa pongezi kwa taasisi hizi kwa kufanya tukio hili kwa awamu ya pili sasa kwani wanahamasisha kwa vitendo utalii wa ndani na nje ya nchi.” Amesema Mh. Malisa.
Akizungumzia tukio hilo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda, amesema tukiweza kuwaelimisha wakazi wa maeneo husika juu ya utalii wa anga na vimondo ni fursa hasa ya utalii kwa wakazi wa maeneo husika na inaweza kuingiza pato kubwa kwa wananchi na serikali.
“Mahali vimondo vilipoangukia ni fursa adhimu kwa biashara ya utalii, nasi (OUT) tunafanya makongamano haya ili wananchi watambue kuwa hii ni fursa kubwa na biashara pia. Lakini pia tunapoalika vijana wadogo kwenye kongamano hizi maana yake tunaandaa vizazi vijavyo vijikite katika utalii wa anga ambao kwa nchini hapa bado upo chini.” Amesema Prof. Bisanda.
Aidha, alisistiza kuwa ili kuimarisha zaidi utalii wa anga Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kipo kwenye mikakati ya kuweka darubini kubwa juu ya kilele cha mlima Kilimanjaro ambayo watalii wataitumia kuangalia anga kwa urahisi na ubora wa hali ya juu.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Uhifadhi kutoka Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro, Inj. Joshua Mwamkunda, amesema wameandaa kongamano hili ili kufikisha ujumbe kwa Watanzania kuwa kimondo ni muhimu hivyo tunapaswa kuutambua urithi wa anga, kuuhifadhi na kuutangaza kwa ajili ya kuutumia kama fursa ya utalii nchini.
“Kimondo ni urithi tofauti na wa kipekee sana, kongamano hili linajadili namna ya kuutambua urithi muhimu uliopo nchini na baada ya hapo ni namna gani tunaweza kuvitumia kama fursa.” Amesema Inj. Mwamkunda.
Kongamano la pili la utalii wa anga lilifanyika Juni 29, ni utangulizi wa maadhimisho ya siku ya vimondo duniani inayoadhimishwa Juni 30 kila mwaka. Hivyo, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wameandaa kongamano hili pamoja na mbio za riadha zinazojulikana kama Mbio za Kimondo zinazotarajiwa kufanyika siku ya maadhimisho ya vimondo duniani mkoani Songwe ambako kimondo kikubwa kuliko vyote nchini kinapatikana.