Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kimezindua Mpango Mkakati mpya wa mwaka 2023-2024 mpaka 2025-2026 katika Baraza la 116 lililofanyika jijini Dodoma tarehe 23 Juni, 2023.
Akiziongoza uzinduzi huo Mwenyekiti wa Baraza Prof. Joseph Kuzilwa ameipongeza Menejimenti ya OUT kwa kufanikiwa kutekeleza kwa mafanikio makubwa mpango mkakati wake unaoishia Juni 30, 2023.
“Napenda kutumia fursa hii kuipongeza Menejimenti ya chuo chini ya uongozi wa Prof. Bisanda kwa kufanikiwa kutekeleza mpango mkakati unaoishia Juni mwaka huu kwa zaidi ya Asilimia Sabini (70%). Hakika ni mafanikio makubwa katika chuo hiki ambayo yameshuhudia uimarishaji wa huduma za kujifunzia na kufundishia kupitia mifumo mbalimbali ya TEHAMA, uundwaji wa sera mbalimbali, kuongezeka kwa udahili, kuimarika kwa miundombinu, maendeleo ya kitaaluma ya wahadhiri na waendeshaji na maendeleo mengine mengi kutaja kwa muhtasari. Ni imani ya Baraza kwamba kuzinduliwa kwa Mpango mkakati huu Mpya kutaongeza chachu ya kufanya kazi kwa bidii zaidi ili utakapokamilika uwe umetekelezwa kwa asilimia nyingi zaidi ya 100.” Amesema Prof. Kuzilwa.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Elifas Bisanda amelishukuru Baraza kwa kupitisha Mpango Mkakati mpya wa miaka 4 ijayo ambapo yeye kama msimamizi na mtendaji mkuu wa OUT atahakikisha unatekelezwa kikamilifu.
“Ndugu Mwenyekiti wa Baraza, napenda kutoa shukurani za dhati kwako na Baraza kwa jumla kwa kupitisha mpango mkakati huu. Ni dhahiri kuwa, Baraza hili ndicho chombo cha juu cha usimamizi wa Chuo na hata mafanikio tuliyoyapata katika mpango mkakati unaoishia Juni 30 ya mwaka huu ni kutokana na usimamizi mzuri wenye viwango vya juu vya Baraza lako. Tutahakikisha mpango mkakati huu mpya nao unatekelezwa vizuri kwa kufanyia kazi maelekezo yote na ushauri kutoka kwenye Baraza lako muda wote wa utekelezaji wake.” Alimaliza kusema Prof. Bisanda.
Naye Mwenyekiti wa timu ya uratibu wa maandalizi ya Mpango Mkakati huo mpya Prof. George Oreku ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Fedha, Mipango na Utawala amelishukuru Baraza kwa kuhitimisha kazi hii ya Mpango mkakati kwa kuupitisha na kisha kuuzindua rasmi.
“Maandalizi ya Mpango Mkakati huu mpya yalianza takribani mwaka mmoja uliopita na umepitia hatua mbalimbali za kushirikisha wadau mpaka leo hii kuzinduliwa. Mpango Mkakati huu umeandaliwa kwa kuzingatia viwango vya mipango mikakati ya Taasisi za Umma uliotolewa na serikali. Hivyo kwa niaba ya timu yote ya uratibu ambayo ilijumuisha vitengo na idara zote za Chuo, napenda kuishukuru Menejimenti kwa kuwezesha kazi hii kukamilika na leo Baraza limeuzindua Mpango Mkakati huu tayari kwa utekelezaji kuanzia Julai 1, 2023.” Alisema Prof. Oreku.
Mpango Mkakati huu ni wa miaka 4 ambapo mpaka kufikia 2026 kutakuwa na dira mpya ya maendeleo ya Taifa na hapo utaandaliwa Mpango Mkakati mwingine ili kwenda sambamba na dira mpya ya Taifa ya maendeleo.