Call: +255 22 2668992

MAKAMU WA RAIS AFANYA ZIARA CHUO KIKUU HURIA CHA TANZANIA.

makamu-wa-rais-afanya-ziara-chuo-kikuu-huria-cha-tanzania

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, amefanya ziara makao makuu ya chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na kusema kuwa chuo hiki ni nafasi adhimu katika kuhakikisha hakuna Mtanzania anakosa fursa ya kujiendeleza kielimu.

Dkt. Mpango, amefanya ziara ya kutembelea makao makuu ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Disemba 12, 2022, Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo amekutana na uongozi wa chuo hiki na kuzungumza na watumishi, wanachuo na viongozi mbalimbali wa kiserikali.

“Chuo hiki kimeweza kutoa nafasi kwa Watanzania wengi kujiendeleza kielimu wakiwamo viongozi mbalimbali, hivyo serikali itaendelea kuboresha chuo hiki na mazingira yake ili kiweze kutoa elimu bora na kuwajengea wahitimu uwezo wa kujiajiri na kushindana kwenye soko la ajira na kushiriki katika fursa mbalimbali.” Amesema Dkt. Mpango.

Aidha, Dkt. Mpango, ametoa maelekezo kwa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, kutoa kipaumbele kwa kukamilisha ununuzi na umiliki wa majengo yaliyopo katika eneo la Kinondoni Biafra yanayotumiwa kama kituo cha mkoa wa Kinondoni. Takriban miaka 20 chuo hiki kimekuwa kikiyapangisha na hivyo kukubaliana na mmiliki kukiuzia chuo hiki majengo hayo.

Katika ziara hiyo, Makamu wa rais amejionea bunifu mbalimbali zinazofanywa na watumishi na wanafunzi wa chuo hiki hivyo kusisitiza bunifu hizo kusogezwa kwa jamii ili kukitangaza chuo hiki kwa kazi inazofanya lakini pia bunifu hizo ziweze kusaidia jamii hizo katika kuleta maendeleo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, akizungumza katika ziara hiyo amesema serikali imekuwa ikitilia mkazo katika swala la elimu na hivyo kutawanya fursa za elimu katika maeneo mbalimbali ya nchini. Katika fursa hizo serikali imekuwa ikijenga vyuo vipya lakini pia kuboresha vyuo mbalimbali kikiwemo Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambacho kimenufaika kupitia miradi mbalimbali ambayo itakiimarisha na kuongeza udahili.

“Msukumo wa serikali unaoonekana haraka ni kuongeza udahili vyuoni. Wakati swala la msukumo wa kuongeza udahili linaendelea hatuna mjadala katika swala la ubora. Tunaongeza umakini mkubwa sana katika namna ya kuhakikisha ubora wa elim ya vyuo vikuu unaimarika na kuongezeka.” Amesema Prof. Mkenda.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Joseph Kuzilwa, akitoa neno a shukrani, amemshukuru Makamu wa Rais, Dkt. Mpango kwa ushauri na maelekezo aliyotoa kwa niaba ya serikali ili kuboresha chuo hiki na kuharakisha maendeleo ya Mtanzania.

Hali kadhalika, Prof. Kuzilwa, amesema kuwa elimu na huduma zinazotolewa na chuo hiki zinapimwa na mamlaka zote za usimamizi wa elimu nchini,  hivyo elimu inayotolewa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania inapimwa na mamlaka hizo za kielimu nchini.

Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Mh. Mizengo Pinda, amesema chuo hiki kimefanya kazi kubwa sana hasa katika kuendeleza watumishi ambao tayari wapo katika ajira. Mh. Pinda, amesema kwamba, Watumishi wengi hasa wa serikali wamekuwa wakijiunga na chuo hiki na kupata maarifa yanayowasidia kuongeza ufanisi zaidi kazini.

“Tofauti na vyuo vingine wao hawafuati wanafunzi ila sisi tunawafuata wanafunzi wetu, tunahitaji umakini fulani ambao tukifanikiwa chuo hiki kitaweza kufanya mambo makubwa.” Amesema Mh. Pinda.

Kwa Upande wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda amesema chuo kina changamoto nyingi lakini moja wapo ni kukabiliana na gharama kubwa za mtandao ambazo ndiyo nyenzo muhimu ya ufundishaji katika chuo hiki. Ameongeza kuwa, Chuo kinatumia zaidi ya bilioni moja kila mwaka kulipia internet na kununua vifaa vya TEHAMA.

Aidha Prof. Bisanda ameishukuru serikali kwa kuelekeza Wizara itusaidie kupata ardhi Dodoma ili chuo hiki nacho kiweze kuhamia makao makuu ya nchi halikadhalika ameiomba serikali kusaidia ujenzi wa vituo vinane vya mikoa iliyosalia, ambavyo ni Tabora, Njombe, Mara, Tanga, Katavi, Pemba, Songwe na Unguja.

“Napenda kuishukuru Serikali yako, chini ya Mheshimiwa Rais Samia Hassan Suluhu, kwa kujumuisha chuo hiki katika mradi wa kuchochea mageuzi ya kiuchumi kupitia elimu ya juu (HEET). Chuo hiki kimetengewa dola million tisa ambazo zitatumika kujenga maabara saba za sayansi za kikanda nchini.” Amesema Prof. Bisanda.

Makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, ametembelea chuo Kikuu Huria cha Tanzania ikiwa na kutimiza ahadi yake ya kukitembelea chuo hiki kabla ya Disemba 30, 2022 aliyoitoa wakati wa mahafali ya 41 yaliyofanyika Novemba 24, 2022 katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza.